Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah A'raafi katika tamko la kimkakati, akielezea masomo sita ya kistaarabu ya Arubaini ya mwaka 1405 H.Sh. na kuhuisha kumbukumbu ya kiongozi shahidi mtukufu wa Umma wa Kiislamu, alisisitiza kwamba: Arubaini ya mwaka huu inaanza chini ya kivuli cha huzuni kubwa lakini yenye fahari; huzuni ya kumpoteza "Imamu Shahidi", marjii huyo mwenye huruma na kiongozi mwenye hekima ambaye aliyatumia maisha yake yenye baraka katika njia ya kuupa heshima Uislamu na Iran; Imamu shahidi ambaye aliishi katika njia ya Imam Hussein (as) na akapata shahada kwenye njia ya Imam Hussein (as).
Ifuatayo ni matini kamili ya tamko hilo muhimu na la kimkakati la Mkurugenzi wa Hawza:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
وَ بَذَلَ مُهْجَتَهُ فِیکَ لِیَسْتَنْقِذَ عِبَادَکَ مِنَ الْجَهَالَهِ وَ حَیْرَهِ الضَّلَالَهِ
(Ziyara ya Arubaini).
Arubaini ya Imam Hussein (as) ya mwaka huu inajitokeza katika upeo mwingine na kwa sura isiyokuwa na mfano ya muunganiko wa mbingu na ardhi. Ni Arubaini ambayo si maombolezo na kuomboleza kwa ajili ya Bwana na Kiongozi wa Mashahidi pekee, bali ni kioo kinachoakisi kwa ukamilifu mwendelezo wa njia ya Ashura hadi zama za sasa; zama ambazo ndani yake hamasa ya Imam Hussein (as) imeunganishwa kwa namna isiyoweza kutenganishwa na hamasa ya uwepo wa wananchi jasiri na wenye heshima wa Iran katika medani.
Mazishi ya kihistoria na yenye utukufu ya mwili mtukufu wa kiongozi huyo shahidi nchini Iran na Iraq; katika miji mitakatifu ya Najaf na Karbala, pamoja na hamasa ya kipekee na ya kihistoria ya wananchi wenye heshima na waaminifu wa Iran na Iraq, yameonyesha kwamba uhusiano wa kina wa Umma wa Kiislamu, hususan wananchi wa Iran na Iraq, na malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu unaendelea kuimarika kila siku.
Kwa upande mwingine, Arubaini hii inafanyika katika medani ya mapambano ya kimaumbile na ya kistaarabu dhidi ya ubeberu duniani, hususan Marekani mhalifu. Ni vita vya mseto ambavyo kwa kiwango kisichokuwa na mfano vimepanuka katika nyanja za kijeshi, kiuchumi na kiutambuzi. Marekani, baada ya kupokea mapigo makali na mafunzo yasiyosahaulika kutoka kwa vikosi vya kijeshi vya Iran, wananchi jasiri wa Iran na mhimili wa Muqawama, imezidi kudhihirisha kushindwa na kukata tamaa kwake.
Sasa, taifa hili la Muqawama, chini ya uongozi wa hekima wa Mtukufu Ayatullah Sayyid Mujtaba Khamenei (Mwenyezi Mungu amlinde), kwa mwongozo wa Marajii wakuu wa Qom na Najaf, na kwa nguvu ya imani na uoni wa wananchi, limesimama kama dola ya Tawhidi isiyoshindikana mbele ya tamaa za kupindukia za adui mwuaji na mhalifu wa Marekani na Uzayuni. Hamasa ya Arubaini ya mwaka huu yenyewe itageuka kuwa jibu thabiti kwa porojo na ndoto hizo za Marekani, na itaandika ukurasa mwingine wa dhahabu wa mngurumo na ufufuo mkubwa wa Umma wa Kiislamu.
Kwa kutambua kwa kina hali hii nyeti, pamoja na upeo mpana na mgumu wa uwanja na medani ya mapambano, na kwa mtazamo wa kimkakati, katika fursa hii adhimu ya Arubaini ambayo ni uwezo wa kipekee kwa ajili ya kubainisha haki na kufanya jihadi ya uelimishaji, napenda kuwasilisha mambo yafuatayo kwenu, enyi wanafunzi wa elimu ya dini, maulamaa na wahubiri watukufu ambao ni wabeba bendera wa elimu, tablighi, uongofu na uelimishaji katika njia hii yenye heshima.
Ninatumaini kwamba kwa kuomba msaada wa Mtukufu Sayyidush-Shuhadaa (as), tutaweza kuitumia fursa ya Arubaini kwa ajili ya kuhuisha kumbukumbu na malengo ya mashahidi, hususan Imam Khomeini Mkuu na Imamu wetu Shahidi, na kubainisha fikra za Mapinduzi ya Kiislamu, Muqawama na kueneza matumaini. Aidha, katika vita hivi vya kila upande vinavyohusu uwepo wetu, tuwe mstari wa mbele kama askari wenye utambuzi na wapiganiaji wa njia ya Mwenyezi Mungu.
1. Hamasa ya Arubaini; Utume Mpya na Ufufuo Mpya wa Umma
Kama inavyobainika kutokana na ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mnasaba wa kumbukumbu ya miaka thelathini na saba ya kufariki kwa Imam Khomeini, kuna matukio matano makubwa katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu ambayo yanaonesha kwa uwazi hakika ya "utume mpya wa Umma":
1. Mapinduzi ya Ashura ya wananchi wa Iran chini ya uongozi wa Imam Khomeini (ra) tarehe 15 Khordad 1342 H.Sh.
2. Mwanzo wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu tarehe 12 Bahman 1357 H.Sh.
3. Kufariki kwa majonzi makubwa kwa mwanzilishi mkuu wa Mapinduzi tarehe 14 Khordad 1368 H.Sh. na kuanza kwa zama mpya chini ya uongozi wenye busara wa Imamu Shahidi.
4. Ushahidi wa kidhulma wa Imamu Shahidi tarehe 10 Esfand 1404 H.Sh.
5. Hamasa ya mazishi ya kihistoria ya Imamu Shahidi nchini Iran na Iraq, ambayo yalileta ufufuo mkubwa na kuionesha dunia kiwango kipya cha utume na uwepo wake wa kushangaza.
2. Umoja, Udugu na Mshikamano wa Umma wa Kiislamu na Mhimili wa Muqawama Kuzunguka Arubaini ya Imam Hussein (as)
Arubaini ya Imam Hussein (as) ni mkusanyiko mkubwa zaidi wa wanadamu katika historia, ambapo mipaka ya kijiografia, kikabila, kilugha na kimadhehebu hupoteza umuhimu wake mbele ya "Mapenzi ya Imam Hussein (as)."
Mkusanyiko huu mkubwa ni mfano halisi wa Aya Tukufu isemayo:
«وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِیعًا وَلَا تَفَرَّقُوا»
Umoja na mshikamano unaojengwa juu ya mapenzi na Wilaya ya Ahlul-Bayt (as) si hisia za kawaida tu, bali ni mkondo unaojenga utambulisho na kuimarisha mshikamano ambao umeufanya mhimili wa Muqawama kuwa mmoja na usioshindika mbele ya adui wa pamoja.
Mtukufu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba: "Mhimili wa Muqawama ni mmoja na wenye mshikamano, na dosari yoyote ndani yake huwanufaisha maadui."
3. Jihadi, Muqawama na Kusimama Imara Chini ya Kaulimbiu ya Ashura: "Mtu kama mimi hawezi kumpa baia mtu kama Yazid."
Kauli yenye moto ya Mtukufu Sayyidush-Shuhadaa (as):
«مثلی لا یبایع مثل یزید»
haikuwa tu kukataa kutoa baia katika tukio la kihistoria, bali ni kanuni ya kimkakati inayofaa kwa zama zote.
Kwa kauli hii, Imam Hussein (as) aliweka mpaka wa milele unaotenganisha kambi ya haki na kambi ya batili. Leo pia kaulimbiu hii ndiyo bendera iliyo juu zaidi ya mhimili wa Muqawama dhidi ya Firauni wa zama hizi, yaani Marekani na vibaraka wake. Na kama vile Yazid hakupata chochote kutokana na kumuua kishahidi Imam Hussein (as) isipokuwa fedheha na udhalili, vivyo hivyo Marekani, kupitia uhalifu wake, haitavuna chochote isipokuwa aibu na kushindwa mfululizo.
4. Arubaini na Wito wa Kisasi na Kudai Damu ya Imamu Shahidi
Hamasa ya Arubaini ya mwaka huu imeungana na hamasa ya kulipiza kisasi cha damu ya shahidi wa njia ya Imam Hussein (as), yaani kiongozi mpiganiaji na shahidi. Pale ambapo katika mazishi yake ya kipekee na ya kihistoria nchini Iran na Iraq ngumi zilipokunjwa na sauti za kulipiza kisasi na kudai damu zilipopaa kutoka vilindini mwa nyoyo za waumini, kwa hakika hilo lilikuwa agano lililowekwa mbele ya Mwenyezi Mungu, Imam Hussein (as) na Imam wa Zama (aj), ambalo limeandikwa katika historia.
Kisasi chetu ni kisasi cha damu ya aliyedhulumiwa dhidi ya dhalimu; kisasi ambacho Mwenyezi Mungu amekiahidi katika Qur'ani:
«وَمَنْ قُتِلَ مَظْلُومًا فَقَدْ جَعَلْنَا لِوَلِيِّهِ سُلْطَانًا»
na leo mwenye mamlaka ya kudai damu hii ni Umma ulioamka na unaotaka kulipiza kisasi; Umma ambao katika mazishi ya Imamu huyo Shahidi uliweka ahadi kwamba hautaacha kudai kisasi mpaka madhalimu, wanyang'anyi na Mayazid wa zama hizi waangamizwe kikamilifu.
5. Hamasa ya Arubaini; Mhimili wa Mshikamano na Kusaidiana katika Maisha na Uchumi, Pamoja na Jihadi ya Kiuchumi katika Ngazi ya Kitaifa na Kimataifa
Katika hali ya sasa ambapo adui ameanzisha vita vya mseto na kupitia vita kamili vya kiuchumi, vikwazo vya kidhalimu na uharibifu wa miundombinu analenga kuwakatisha tamaa wananchi, mshikamano, kusaidiana kwa waumini na upangaji wa taasisi husika kwa kuzingatia jihadi na Muqawama wa kiuchumi ndiyo silaha kubwa zaidi ya Umma wa Kiislamu.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:
«مَثَلُ الْمُؤْمِنِينَ فِي تَوَادِّهِمْ وَتَرَاحُمِهِمْ وَتَعَاطُفِهِمْ مَثَلُ الْجَسَدِ الْوَاحِدِ إِذَا اشْتَكَى مِنْهُ عُضْوٌ تَدَاعَى لَهُ سَائِرُ الْجَسَدِ بِالسَّهَرِ وَالْحُمَّى»
Waumini katika kupendana, kuhurumiana na kushikamana wao kwa wao ni kama mwili mmoja; kiungo kimoja kinapoumia, mwili mzima huathirika kwa kukosa usingizi na kwa homa.
Waumini hushirikiana katika furaha na huzuni, na kamwe hawapuuzi majonzi na mateso ya ndugu zao. Hii ndiyo roho inayotawala hamasa ya Arubaini; mahali ambapo kuwahudumia mazuwari kunafuta kila hesabu ya kimada, na waumini hawasiti kutumia hata kile kidogo walicho nacho ili kukidhi mahitaji ya wengine.
Kwa hiyo, Arubaini ndiyo fursa bora zaidi ya kuonesha kwa vitendo mshikamano na kusaidiana katika nyanja ya maisha na uchumi, na inaweza kuifanya dhana ya uchumi wa Muqawama kuwa halisi kwa maana yake kamili.
6. Arubaini; Mazoezi ya Kivitendo ya Kujiandaa kwa Ajili ya Kudhihiri kwa Imam Mahdi (aj)
Wakati huo huo, serikali na mataifa ya Kiislamu vinapaswa kushiriki katika jihadi kubwa ya kiuchumi kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa ulimwengu wa Kiislamu na kujenga nguvu mpya ya kiuchumi kwa ushirikiano wa wananchi na wasomi.
Arubaini ya Imam Hussein (as) si mkusanyiko mkubwa wa maombolezo pekee, bali ni mazoezi ya kivitendo ya kuunda Umma mmoja na maandalizi ya utekelezaji wa serikali ya kimataifa ya Mtukufu Imam wa Zama (aj). Wakati ambapo mamilioni ya watu, kwa moyo mmoja na sauti moja, husafiri kutoka pembe mbalimbali za dunia kuelekea Karbala, kwa hakika wanaufufua kwa kiwango kidogo Mapinduzi ya Sahibuz-Zaman (aj). Mwafaka huo mkubwa ni bishara ya kuchomoza kwa ahadi ile ambayo ndani yake:
«یَمْلَأُ الْأَرْضَ قِسْطًا وَعَدْلًا»
yaani, ataujaza ulimwengu kwa uadilifu na haki, na atawakusanya wanadamu wote chini ya hema la uadilifu na maarifa.
Imamu wetu Shahidi alitumia maisha yake yote katika njia ya kutimiza ahadi hii, na kwa damu yake safi akaandika jina lake miongoni mwa wasaidizi wa Mtukufu Imam Mahdi (aj) na miongoni mwa wale waliojitolea mhanga katika njia ya kudhihiri kwake.
Leo hii, Arubaini ni daraja linalounganisha damu ya Imam Hussein (as) na damu ya Imamu Shahidi kuelekea upeo wa kudhihiri kwa Imam Mahdi (aj). Kwa sababu kadiri mikusanyiko hii inavyozidi kuwa na hamasa, mshikamano na malengo ya wazi, ndivyo maadui wa haki wanavyozidi kudhoofika na mazingira ya kudhihiri Imam Mahdi (aj) yanavyokuwa mepesi zaidi.
Maoni yako